Pages

Tuesday, February 25, 2014

Maandalizi ya Tamasha la Kimataifa la 33 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo Septemba 2014 yaanza mapemaaaa!

Na Andrew Chale, Bagamoyo 
TAMASHA la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambalo kwa mwaka huu (2014) litakuwa la 33, ambapo linatarajia kulindima kwa siku saba, kuanzia Septemba 22 hadi 28, kwenye viunga vya Chuo cha Sanaa Bagamoyo. 
 Tamasha hilo la 33, mwaka huu, lenye kauli mbiu, “Sanaa na Utamaduni katika kukuza Utalii”, limekuwa msaada mkubwa kwa wasanii na vikundi mbali mbali kujitangaza kitaifa na kimataifa pamoja na kutoa fursa za kibishara katika kipindi chote cha tamasha. 

 Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Abraham Bafadhil ‘Bura’, alieleza kuwa, tayari mipango na maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea katika kufikia malengo huku akiwaomba wadau kujitoakeza na kudhamini tamasha hilo. 


 “Milango ipo wazi hivyo, kwa wadhamini kujitokeza na kuchangamkia fursa hii hadimu, kwani tamasha hili ni kongwe katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Afrika kwa ujumla” alisema Bura, na kuongeza kuwa, tamasha hilo lenye mvuto wa kipekee ndani na nje ya Tanzania, limekuwa likipata umaarufu mkubwa kila mwaka kutokana na idadi kubwa ya watazamji wa ndani na wale wa kutoka Mataifa mbali mbali duniani. 


 Kwa upande wake, Katibu wa tamasha hilo, Benjamini Mahimbali alieleza kuwa, tamasha hilo limekuwa na mafanikio ikiwemo ongezeko kubwa la watazamaji na vikundi vinavyoomba kufanya maonyesho.

 “Idadi ya watazamaji na imekuwa ikiongezeka kila mwaka, huku kwa mwaka jana tulikuwa na wastani wa watazamaji elfu nne mia saba kwa siku (4,700), ikiwemo wa rika zote.” Alisema Ben, na  kuongeza kuwa, wanatarajia ongezeko hilo kuwa kubwa zaidi kutokana na maboresho na mipango mbali mbali inayotarajiwa kufanyika mwaka huu. 


 Katika tamasha hilo maonyesho mbali mbali yanatarajiwa kuonyeshwa ikiwemo; Muziki wa aina tofauti, ngoma, maigizo, sarakasi, mazingaombwe na maonyesho kemkem ya sanaa na utamaduni wa Mtanzania na ya Mataifa mengine duniani. 


 Kwa upande wa fomu za kushiriki tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu wanatarajia kupokea vikundi zaidi ya 40, zinatarajiwa kutolewa kwenye ofisi za Chuo hicho pamoja na tovuti ya chuo (www.tasuba.ac.tz) 
 Au Kwa mawasiliano na maulizo juu ya ushiriki na udhamini waweza kufika Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TaSUBa) au kupitia namba;
 +255(0) 715 472 745 
+255(0) 655 840 405
 +255(0) 754 310 425 
+255(0) 712 683 408 

No comments:

Post a Comment